Maangamizi ya Waarmenia

Maangamizi ya Waarmenia (kwa Kiarmenia Հայոց Ցեղասպանություն, Hayots Tseghaspanutyun) maarufu kwa Kiingereza kama Armenian Holocaust,, Armenian Massacres na kwa Kiarmenia Մեծ Եղեռն, Medz Yeghern, "Ovu kubwa"), yalikuwa sera ya Dola la Osmani ya kukomesha Waarmenia wote walioishi ndani ya eneo la dola hilo (leo nchini Uturuki. Makadirio ya waliouawa ni kati ya watu milioni 1 na 1.5. Tarehe inayohesabiwa kuwa mwanzo wa hayo mauaji ya kimbari ni 24 Aprili 1915, ambapo watawala Waturuki waliteka wasomi Waarmenian 250 mjini Istanbul. Tarehe hiyohiyo miaka 100 baadaye yalifanyika maadhimisho makubwa katika nchi mbalimbalimbali, hasa huko Etchmiadzin, makao makuu ya kiroho ya Waarmenia, ambapo Patriarki Katolikosi Karekin II aliwatangaza kwa jumla waliouawa kuwa watakatifu wafiadini. Maangamizi yalitekelezwa kwa awamu mbili: kwanza wanaume wazima waliuawa mara moja au kulazimishwa kufanya kazi za shokoa, halafu wanawake, watoto, wazee na wagonjwa waliswagwa na wanajeshi hadi jangwa la Syria ili wafe njiani, baada ya kunyimwa chakula, maji, mbali ya kuibiwa, kubakwa na kuuawa. Makabila mengine pia, hasa ya Kikristo, kama vile Waashuru na Wagiriki, waliangamizwa na Waturuki wakati huohuo. Mtawanyiko wa Waarmenia duniani unatokana kwa kiasi kikubwa na mauaji hayo. Vilevile ni kutokana nayo kwamba Raphael Lemkin alitunga neno genocide mwaka 1943 kama maangamizi ya halaiki ya mpango na kadiri ya sera. Maangamizi hayo yanahesabiwa ya kwanza katika karne ya 20 yakifuatwa na yale makubwa zaidi ya maangamizi makuu dhidi ya Wayahudi wa Ulaya chini ya Adolf Hitler. Uturuki, ulioshika nafasi ya Dola la Osmani, unazidi kukataa neno genocide kuhusiana na mauaji ya Waarmenia, ingawa wataalamu wengi wa historia wanaliona kuwa sahihi na nchi nyingi zaidi na zaidi zinaudai ukiri kosa na kupatana na Waarmenia.


© MMXXIII Rich X Search. We shall prevail. All rights reserved. Rich X Search